Ijumaa 17 Julai 2026 - 18:00
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Katika Mkutano na Wanafunzi wa Hawza ya Karbala: Asisitiza Kuendelezwa Njia ya Mashahidi na Nafasi ya Wanafunzi Katika Kueneza Mafundisho ya Ahlul-Bayt (as)

Hawza/ Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, katika mkutano wake na kundi la wanafunzi wa harakati hiyo wanaosoma katika Hawza ya Karbala Tukufu, alisisitiza kuwa; njia ya mashahidi ndiyo njia ya heshima na ushindi wa Uislamu. Alisema kuwa maadui hudhani kwamba kwa kuwaua viongozi wakubwa wa dini wanaweza kuuangamiza Uislamu na madhehebu yake, ilhali shahada huyafanya malengo na misingi ya dini kuwa hai zaidi na husababisha kuenea kwa njia hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, jioni ya Jumanne tarehe 29 Muharram 1448 Hijria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, alikutana na kufanya mazungumzo na kundi la wanafunzi na watafiti wa harakati hiyo wanaoendelea na masomo katika Hawza ya Karbala Tukufu nchini Iraq.

Katika mkutano huo, Sheikh Zakzaky alizungumzia kuuawa kishahidi Ayatullah al-Udhma Sayyid Khamenei (qs), akieleza kuwa kuafikiana kwa tukio hilo na mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwezi aliopata shahada Amirul-Muuminina Imam Ali (as), pamoja na mazishi yake kufanyika katika usiku wa kumbukumbu ya shahada ya Imam Zayn al-Abidin (as), ni miongoni mwa vielelezo vya hekima ya Mwenyezi Mungu. Alisisitiza kuwa matukio hayo si ya bahati mbaya, bali yanaonesha mwendelezo wa njia ya shahada, njia ambayo maadui hawawezi kufahamu hakika yake.

Aliendelea kusema kuwa; maadui daima hudhani kwamba kwa kuwaua viongozi wakubwa wa dini wanaweza kuidhoofisha dini ya Mwenyezi Mungu. Katika muktadha huo alikumbusha maneno aliyowahi kuwaambia baadhi ya viongozi wa vyombo vya usalama baada ya tukio la Zaria, akisema: "Kama shahada ya mtu mmoja ingeweza kuangamiza madhehebu ya Shia, basi mtu wa kwanza ambaye angepaswa kufanya hivyo ni Imam Hussein (as). Lakini shahada yake ndiyo iliyosababisha madhehebu haya kuenea zaidi na kuimarika zaidi."

Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alisisitiza kuwa; huu ni utaratibu wa Mwenyezi Mungu unaoendelea hadi leo, na kwamba kila jitihada za maadui za kuizima nuru ya haki zitatoa matokeo yaliyo kinyume na matarajio yao. Aliongeza: "Walidhani kwamba kwa kuuawa kishahidi Sayyid Khamenei kila kitu kingefikia mwisho, lakini ukweli ni kwamba shada hiyo umelifanya jina lake, fikra zake na njia yake kuwa hai zaidi kuliko hapo awali."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Zakzaky akiwahimiza wanafunzi kutumia kikamilifu fursa ya kusoma elimu za dini alisema: "Mmefika katika ardhi hii kwa ajili ya kujifunza maarifa ya Ahlul-Bayt (as), ili mtakaporudi katika nchi zenu muwanyweshe kiu ya maarifa ya Kiislamu wale wanaoyahitaji. Kwa sababu watu wa maeneo yetu leo wanahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuyafahamu mafundisho ya Ahlul-Bayt (as)."

Akizungumzia miaka mingi ambayo wananchi wa eneo hilo walinyimwa fursa ya kuyafikia mafundisho halisi ya Ahlul-Bayt (as), alisema kwamba; licha ya vikwazo vyote, mwelekeo wa watu kuelekea mafundisho hayo unaendelea kuongezeka siku baada ya siku.

Sheikh Zakzaky pia alikumbusha uimara na kujitolea kwa Amirul-Muuminina Imam Ali (as) pamoja na wafuasi wake wa kweli katika historia, akisisitiza kuwa; heshima ya kweli hupatikana kwa kusimama imara katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kwamba mashahidi huendelea kuwa na athari kubwa zaidi katika jamii hata baada ya kufariki kwao. Katika muktadha huo alimrejelea Shahidi Sayyid Qaid, akisema kuwa watu wengi waliitambua zaidi nafasi na ukubwa wa shakhsia yake baada ya kuuawa kishahidi.

Mwishoni mwa hotuba yake, Sheikh Zakzaky alisema kuwa, njia ya kujitolea na kujitoa muhanga ndiyo njia pekee ya kufikia ushindi. Alisema: "Yeyote anayesema kuna njia rahisi zaidi kuliko kujitolea na kusimama imara, anapaswa kujua kwamba kama njia hiyo ingekuwapo, basi Imam Hussein (as) na masahaba wake wangeichagua. Ushindi unapatikana kwa kusimama imara katika njia ya Mwenyezi Mungu na kujisalimisha mbele ya mapenzi Yake."

Akimalizia, alieleza matumaini yake makubwa kuhusu mustakabali wa njia hiyo na kusema: "Tuna yakini kwamba hatutashindwa kamwe, kwa sababu tuko pamoja na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mtoaji wa ushindi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha